Shuta alimhimiza dereva wake aendeshe gari lake kwa kasi. Dereva alivurumisha gari kwa kasi ajabu. Magurudumu yakiwa hayaumani, yakatifua vumbi ungedhani ni mashindano ya magari. Walifululiza moja kwa moja kupitia kwa baraste ya vichochoro kuelekea Mto Megwa.
Akiwa yeye ndiye aliyebebwa na aliye kiini cha safari hii, Jera alijishughulisha na mbinu za kujitanzua. Itakuwaje? Kujifanya tu mfu hakutakuwa mwisho! Haya majanadume yanaweza yakampiga marisasi kadhaa. Alighadhabika kwa kushindwa kupata suluhu. Angejiokoa vipi kutoka mikononi mwa majambazi hawa?
Mara kwa ghafla, gari likapunguza kasi na kuegeshwa. Waliokuwa mle ndani walichomoka na kuanza kunong'onezana. Alijaribu kuyarefusha masikio yake asipate kusikia hata kidogo. Akajiweka tayari kwa pigano la maisha yake. Mwokozi wa maisha yake alikuwa nani kama si yeye? Alijiangalia mkononi na kutabasamu. Bahati gani aliyokuwa nayo! Hapo alihisi uwepo wa Mungu kwa kazi yake.
Walikuwa wamembeza kiasi cha hoja. Achukuliwe kama mateka kisha asifungwe? Walimwona vipi hawa? Kwani yeye hajiwezi? Alijicheka kwa kujiona duni. Mwanamume kama yeye kudharauliwa? La hasha! Angewafunza adabu hawa waliombeza.
Mara mlango ulipofunguliwa , Jera aliruka nje na hakuambiwa cha kufanya. Alimshambulia aliyeufungua mlango kwa mateke na mandondi mazito mazito. Kwa kuwa mwana mieleka hodari, alimfadhaisha adui wake. Akawa amepata kifungua kinywa asijue kishuka kilikuwa ki njiani chaja! Baada ya kumweza wa kwanza akajipa kwa wa pili na vivyo hivyo baada ya muda mfupi akawa amemfanyia yale yale aliyokuwa amemfanyia wa kwanza.
Akiwa mwenye furaha alijiona shujaa kwa kuwapiga majambazi wale. Kustaajabia alikuwa akipigiwa makofi na Shuta. Jera akatabasamu. "Heko kaka! Nimependezwa na mienendo yako ya kupigana! Hivi kwamba ulijifunzia wapi?" Shuta aliendelea kuropoka kama kasuku. Naye Jera kwa kushangaa akamtumbulia macho tu, asiseme lolote. "Wacha pia nami nione iwapo mafunzo yangu yalikuwa ya bandia kama ya hawa!" Shuta aliyasema haya huku akiruka kichwangomba hadi alikokuwa Jera. Jera akasonga nyuma . Akampima na kuona kuwa angempiga ngumi za haraka haraka afe naye aende zake kujishughulisha na upelelezi wake.
Jera akawa wa kwanza kukunja ngumi huku Shuta akimtazama kwa dharau. Jera alitayarisha mguu na ngumi kwa wakati mmoja akiwa na nia ya kumshtua na kumgonga mara moja. Alipovurumisha teke na kutupa ndondi mtawalia, alishangaa upeo wa kushangaa alipokutanisha mkonowe na ule wa Shuta. Teke alilokuwa amelituma shingoni mwa Jera likatekwa bakunja na kuinuliwa juu.
Kama hangekuwa amezoea mazoezi aina hii, angepasuka msamba. Kwa vyovyote vile alijizatiti kumpiku Shuta. Ikawa yeye alikuwa anamfanyisha Shuta mazoezi kwa maana Shuta aliyakwepa mateke yake yote. Alipochoka akawa amemruhusu Shuta kuyatuma yake yaliyokuwa na uhakika na shabaha zaidi. Mengi yalimpata ilhali kunayo machache yaliyomkosa. Hata kwa yale yaliyomkosa yalimwumiza kiasi cha kufuja damu mdomoni na kipajini.
Jitu likasonga nyuma na kumpigia Jera makofi. Likacheka na kumwambia, "Nikimalizana na wewe nitamfanyia vivyo hivyo mpenzi wako. Itasemekana mliuana wenyewe kwa wenyewe."
Jera aliyapepesa macho yake kushoto akamwona Shauku amefungwa kwenye gari. Shauku akamlilia amsaidie. "Tafadhali nisaidie." Kilio cha Shauku kilimwondolea maumivu Jera akajikakamua kupigana. Alijipanga sawa sawa na kuyaamrisha makonde ya ufundi kumwangukia Shuta. Shuta aliona teke, akilihepa ndondi ya kooni ikampata sawa. Jera akamchangamkia Shuta. Akampiga sana hadi akadhani amemshinda nguvu alipoanguka.
Akamkimbilia Shauku na kumkata kamba. Akambusu. Akambeba na kumweka garini. Baada ya kuufunga mlango kwa nje, akajiona amenyanyuliwa juu na kutupwa chini. Angalikuwa hajasomea mieleka angalivunjika vipande. Ghafla kama umeme, akateremshiwa mateke mengi kwa mpigo. Mengi yakampata na akawa hana budi ila kutafuta hifadhi mtini. Wakawindana kama wanyama wa mwituni na walipopatana Jera akawa amepata kisiki.
Akakizungusha kisiki na kumtwanga nacho begani . Shuta alijisingizia kutosikia uchungu lakini mipigo ilipozidi ilibidi ajikune apatapo. Akawa amezidiwa maarifa. Hakuweza kuamini kuwa yeye pwagu alikuwa amempata pwaguzi.
Alipokuwa akiendelea kupigana na jitu, akasikia sauti ya Shauku ikionya, "Toka!" Alitazama na kuruka mbali akimwacha Shuta kubondwa na gari alilokuwa akiliendesha Shauku. Ukawa ndio mwisho wa Shuta.
Jera alimwangalia Shauku na kushangaa. Alikuwa amestaajabia ya Musa alipokuwa ametiwa mikononi mwa magaidi ilhali sasa aliyaona ya Firauni alipomwona Shauku akimgonga Jera kwa gari .
"Wewe ni nani?" Shauku aliulizwa. "Shauku!" Akajibu . "Yaonekana una mengi nisoyajua!" "Mengi kama yepi ?" "Mbona ukanifunga ?" "Kwa sababu nilitaka pesa." "Pesa? Pesa zikufanye umsaliti rafiki?" "Nilijua hakuna kingetokea. Nilikuwa nimekuona wewe si wa kuchezea!" "Alah! Ningeuawa ungefanya nini?" "Ingekuwa tu ni mojawapo ya bahati mbaya zilizowahi kunikumba!" "Huna utu!" "Una uhuru gani wa kunihukumu?" "Aliye na utu hamsaliti mie shujaa wa mdomo tu!" "Usidhani utanidanganya muda mrefu- najua wewe ni askari kanzu!" "Nani amesema?" "Hii hapa!"
Jera alionyeshwa mkanda wa kurekodi sauti akaingiziwa kwenye mkanda wa gari wa kucheza nyimbo. Alishangaa aliposikia akihojiwa moja kwa moja na Shauku. Kumbe Shauku alikuwa kachero! Mazingaombwe! Alijilaani kwa kumfikiria vibaya Shauku!
Lakini swali kuu likiwa aliporekodiwa alikuwa amepewa nini hadi akafichua siri kwa asiyemjua? Lazima angepata ukweli wa mambo! Aliapa!
TEGEA SEHEMU YA KUMI